1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalam TZ walalamikia kukosekana sera ya Akili Mnemba

21 Mei 2024

Watalaamu na wanasiasa Tanzania wanaonya kuhusu kuendelea kukosekana kwa sera ya kimkakati wakati dunia ikiendelea kubobea na kujikita katika teknojia ya akili ya kubuni (AI).

https://p.dw.com/p/4g6G1
Afrika |Mkutano wa kilele wa kidijitali mjini Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa na Waziri wa mawasiliano Nape NnauyePicha: Florence Majani

Wakati matumizi ya teknolojia hiyo yakianza kuwavutia wengi ikiwamo vijana wanachipua katika elimu ya vyuo vikuu kumekuwa na wasiwasi kutokana na serikali kutoweka bayana kuhusu sera inayoangazia eneo hilo.

Hatua hiyo inakuja wakati mjadala kuhusu matumizi ya teknolojia hiyo ukiwa umeanza kuchomoza katika maeneo mbalimbali ikiwamo mijadala ya wasomo pamoja na wabunge bungeni inayoendelea kushuhudiwa wakati huu.

Uwepo wa mijadala ya teknolojia

Baadhi wa wasomi wanasema ni muhimu kwa serikali kutambua umuhimu wa kuharakisha sera hasa kwa kuzingatia wingi wa mijadala inayoendelea kugubika kuhusu suala hilo huku sehemu kubwa yao wakianza kuonyesha wasiwasi wa teknojia hiyo kusambaa kwa haraka kwa watumiaji ilhali kukiwa hakuna kanuni wala sera.

Nembo ya Microsoft na Akili Mnemba
Nembo ya Microsoft na Akili MnembaPicha: Andre M. Chang/ZUMA/picture alliance

Mtaalamu wa masuala ya tehama kutoka chuo kikuu cha Dodoma, Dkt Dr Japhera Matogoro anasema kuwapo kwa mijadala inayolenga teknolojia hiyo ni ishara tosha juu ya haja ya kupatikana sera juu ya jambo hilo.

"Ni kweli kuna changamoto ya kutokuwa na sera hasa katika nchi yetu ya Tanzania. Na binafsi niwapongeza wabunge, wananchi na wasomi kwa namna ambavyo wameibua mijadala mizito lakini hii yote ni kuonyesha kwamba watu wako tayari na pengine sasa kuendelea kuwaelimisha na hatimaye tuweze kuja na majibu yataweza kuondoa duku duku juu ya teknolojia hii.," alisema Dkt Mbogoro.

Wanasiasa wamekuwa sehemu kubwa kuchagiza umuhimu wa kuwepo sera rasmi ya kuratibu matumzii ya akili ya kubuni wakihofia huenda wakajikuta wakiandamwa na matukio ya kughushi wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na ule uchaguzi mkuu.

Serikali yalenga kupatikana sera

Akizungumzia suala hilo, mbunge wa viti maalumu, Neema Lugangira anasema ni muhumu mamlaka za utendaji zikatoa uzito kuhusu utungaji wa sera na kanuni zake ili kutua usawa kwa watumiaji wa teknolojia hiyo pamoja na wazalishaji wake.

Logos verschiedener ChatGPT-Apps
Nembo za App tofauti za ChatGPTPicha: Friedrich Stark/epd-bild/picture alliance

"Sasa zinapokuja haya matumizi ya teknolojia kwa bahati mbaya sana kati ya waathirika wakubwa watakuwa ni sisi wanawake katika siasa," alisema Lugangira.

Hata hivyo, waziri wa habari teknolojia na mawasiliano Nape Nauye ameliambia bunge hivi karibuni kuhusu shabaha ya serikali kufanikisha upatikanaji wa sera hiyo katika miezi ya hivi karibuni.

"Tuko tayari na mimi kama waziri kutumia mamlaka ya kisheria kutengeneza kanuni," alisema Nape.

Ingawa teknolojia ya akili ya kubuni imeanza kupewa mwamko mkubwa katika siku za hivi karibuni nchini Tanzania, lakini matumizi yake duniani yamekuwa yakitanuka tangu mwongo mmoja uliopita.