1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UM wahofia kusambaratishwa mkataba wa amani Colombia

Mohammed Khelef
24 Novemba 2021

Umoja wa Mataifa umeonesha wasiwasi kwamba bado kuna makundi na watu wanaohatarisha makubaliano ya amani ya mwaka 2016 kati ya serikali ya Colombia na kundi la FARC, huku Marekani ikiliondowa kundi hilo kwenye ugaidi.

https://p.dw.com/p/43P4e
Kolumbien UN-Generalsekretär Antonio Guterres
Picha: Luisa Gonzalez/REUTERS

Akizungumza baada ya kutembelea kambi inayowahifadhi waasi wa zamani wa kundi la FARC, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema ingawa serikali imekuwa ikichukuwa hatua kadhaa kuhakikisha mkataba huo wa amani unafanikiwa, bado kunahitajika msaada zaidi wa serikali kuhakikisha maisha ya wapiganaji wa zamani wa waasi hayaharibiki. 

Katika kambi hiyo kwenye jimbo la Antioquia, Guterres aliyeambatana na Rais Ivan Duque wa Colombia alishuhudia hali halisi wanayokabiliana nayo wapiganaji hao wa zamani, na akaelezea kusikitishwa kwake na taarifa kwamba wale aliowaita maadui wa amani, wanawaandama walioamua kuutekeleza mkataba wa mwaka 2016 kwa vitisho, utekaji na hata mauaji.

Kolumbiens EX-Präsident Juan Manuel Santos und Chef der FARC Rodrigo Londono Echeverry alias "Timochenko"
Siku mkataba wa amani wa Colombia ulipotiwa saini tarehe 24 Novemba 2016 mjini Bogota. Kushoto ni rais wa wakati huo wa Colombia, Juan Manuel Santos, na kulia ni mkuu wa kundi la FARC, Rodrigo Londono Echeverry. Picha: Mauricio Duenas Castaneda/EFE/dpa/picture alliance

"Nimepatwa na wasiwasi niliposikia maeneo kadhaa bado yanakabiliwa na athari za ukosefu wa usalama. Matendo ya makundi haramu yenye silaha na mauaji ya viongozi, wapiganaji wa zamani na watetezi wa haki za binaadamu yanayapoteza matumaini ya watu. Amani ya Colombia inahitajia kwanza amani ya kwenye mikoa. Na nawanasihini mutumie fursa hii ya kihistoria kuigeuza hamu ya kuwa na amani kuwa ukweli," alisema Guterres.

Marekani yaiondowa FARC kwenye ugaidi

Wakati huo huo, utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani umeliarifu bunge la nchi hiyo kwamba unaliondowa kundi la FARC kwenye orodha ya makundi ya kigaidi, miaka mitano baada ya mkataba huo wa amani kutiwa saini, kwa mujibu wa afisa mmoja wa Congress ambaye hakutaka kutajwa jina. 

Msemaji wa Wizara ya Nje ya Marekani, Ned Price, amethibitisha kwamba serikali imeliarifu bunge hilo juu ya hatua inayotaka kuchukuwa kuhusiana na kundi la FARC, ingawa hakufafanuwa hatua yenyewe.

Kolumbien Präsident Ivan Duque
Rais Ivan Duque wa Colombia akizungumza kwenye kambi ya mafunzo na ujumuishaji inayowahifadhi wapiganaji wa zamani wa kundi la FARC katika mji wa Dabeiba, jimbo la Antioquia, Colombia, siku ya Jumanne (23 Novemba 2021).Picha: Joaquin Sarmiento/AFP/Getty Images

Uamuzi wa kuiondowa FARC kwenye orodha ya magaidi inayawezesha sasa makampuni ya Kimarekani kuwaajiri waliowahi kuwa wapiganaji wa kundi hilo kwenye shughuli zake, zikiwemo za kusaidia uteguwaji wa mabomu ya ardhini yaliyotegwa na kundi hilo katika siku zao za mapambano dhidi ya serikali kuu mjini Bogota.

Kundi la FARC lilisaini makubaliano ya amani na serikali mwaka 2016 yaliyopelekea wapiganaji wake 13,000 kuweka silaha zao chini na kujiunga kwenye makambi ya kuwaandaa kurudi katika maisha ya kawaida. 

Makubaliano hayo ndiyo yaliyomaliza mzozo huo ambao hadi hapo ulishasabisha vifo vya watu 260,000 na kuwafanya mamilioni kuwa wakimbizi. 

Kwa sasa, FARC ni chama cha kisiasa chenye viti vya uhakika kwenye bunge la Colombia.