1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Mazungumzo ya amani katika ukanda wa Gaza yakwama

Tatu Karema
6 Machi 2024

Kundi la wanamgambo la Hamas leo limedumisha msimamo wake wa masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza na kubadilishana mateka na Israel.

https://p.dw.com/p/4dEhQ
Wapalestina wakiangalia uharibifu baada ya Israel kushambulia jengo la makaazi katika eneo la Rafah, Ukanda wa Gaza.
Wapalestina wakiangalia uharibifu baada ya Israel kushambulia jengo la makaazi katika eneo la Rafah, Ukanda wa Gaza.Picha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

Hii ni baada ya Marekani kusema mazungumzo ya mapatano mjini Cairo nchini Misri sasa yamo mikononi mwa kundi hilo.

Katika taarifa, kundi hilo limesema kuwa limeonyesha kuwa tayari kufikia hali ya kukomesha kikamilifu uchokozi dhidi ya watu wake lakini Israel bado inakwepa masharti yake ya makubaliano.

Soma pia: Juhudi za kusitisha mapigano Ukanda wa Gaza zaendelea

Akilitaka kundi hilo la Hamas kukubali masharti yaliyopo mezani, Rais wa Marekani Joe Biden, alisema jana kwamba Israel inatoa ushirikiano na pendekezo mwafaka lilikuwa limetolewa kwa ajili ya kusitisha mapigano kwa kubadilishana na kuachiwa huru kwa mateka wa Israel.

Hamas imeahidi kuendelea kushiriki katika mazungumzo hayo ya Cairo, lakini maafisa wake wamesema lazima kuwa na usitishaji mapigano kabla ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel na kwamba lazima Israel iondoke Gaza na wakazi wote wa  Gaza kuweza kurejea katika makazi yao waliyolazimishwa kuyakimbia.