Umoja wa nchi za Kiarabu, Arab League, umeutaka ujumbe wake wa uangalizi kuondoka nchini Syria. Hayo yamethibitishwa na makao makuu ya umoja huo mjini Cairo, ambapo mataifa kadha ya Kiarabu kutokana na kuendelea kwa ukandamizaji wa serikali ya nchi hiyo dhidi ya wapinzani yameomba kuondolewa kwa waangalizi wake. Waangalizi hao waliingia nchini humo mwezi Desemba kwa masharti ya kuangalia kuondoshwa kwa jeshi katika miji na kuachiliwa huru kwa wafungwa wote wa kisiasa nchini humo. Kwa mujibu wa wanaharakati, jeshi la Syria kwa muda wa siku ya tano mfululizo limepambana na waasi katika mji wa Homs. China na Urusi zimepinga azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa , lililokuwa na lengo la kuilazimisha serikali ya nchi hiyo kuacha kupambana na wapinzani. Shirika linalochunguza ukiukaji wa haki za binadamu nchini Syria limesema kuwa kutokana na mashambulio ya risasi na makombora katika maeneo yanayoishi watu, watu kadha wameuwawa. Katika mapambano dhidi ya mji wa Homs tangu mwishoni mwa juma zaidi ya watu 200 wameuwawa.
Viongozi wa serikali ya muungano nchini Ugiriki wanatayarisha jibu lao kuhusiana na mswada wa kubana zaidi matumizi , ambapo wakopeshaji wanadai ili kuweza kuidhinisha kiasi cha euro bilioni 130 za uokozi ambazo zitaisaidia nchi hiyo kuepuka uwezekano wa kushindwa kulipa madeni yake mwezi ujao. Uamuzi utatangazwa katika mkutano na waziri mkuu Lucas Papademos, ambao ulipangwa kufanyika mchana wa leo na kuahirishwa. Hii itatoa kwa vyama vitatu vinavyounda serikali muda zaidi kupitia waraka wenye kurasa 50 , ambao umetayarishwa na wataalamu wa kundi linaloidai nchi hiyo jana Jumanne. Bila ya kupata mkopo huo , Ugiriki haitakuwa na fedha za kutosha kulipia faida kwa walionunua dhamana mwezi ujao, na kuzusha hali ya kushindwa kulipa madeni na kufilisika na kuleta hali ya mtikisiko katika masoko ya fedha pamoja na uchumi wa dunia.
Male. Waungaji mkono wa rais wa zamani wa Maldive , Mohammed Nasheed, wamefanya ghasia mitaani katika mji mkuu wa nchi hiyo leo wakiwarushia polisi mabomu ya petroli. Wanadai rais huyo arejeshwe madarakani. Ghasia hizo zilizuka baada ya mtu aliyechukua nafasi ya Nasheed , rais Mohammed Waheed Hassan , kutoa wito kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kumaliza mzozo wa kisiasa ambao umeivuruga nchi hiyo kwa miezi kadha sasa. Nasheed amesema kujiuzulu kwake jana Jumanne ilikuwa ni mapinduzi na kwamba ameondolewa madarakani baada ya kulazimishwa kwa mtutu wa bunduki. Ametaka rais mpya Hassan, ambaye alikuwa makamu wake, ajiuzulu, na kwamba atapambana ili kurejea madarakani. Nasheed amewaambia waungaji wake mkono wapatao 2,000 kuwa atarejea madarakani na hatakubali mapinduzi hayo. Na baada ya hapo aliongoza maandamano mitaani. Polisi walijibu kwa kufyatua mabomu ya kutoa machozi na kuwakamata wabunge wawili kutoka chama cha Nasheed.
Majaji nchini Misri wanaochunguza upataji fedha kutoka nje kinyume na sheria wa mashirika yasiyo ya kiserikali , wameyashutumu makundi ya kigeni na ya ndani , ikiwa ni pamoja na yale ya Marekani kwa kuingilia kinyume na sheria masuala ya kisiasa nchini humo. Jaji Sameh Abu Zeid amewaambia waandishi habari leo kuwa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanafanya kazi bila kibali , na kazi zao zinahusiana moja kwa moja na masuala ya kisiasa na sio masuala ya kijamii. Jaji huyo amesema msako uliofanywa Desemba mwaka jana dhidi ya ofisi 17 za mashirika ya ndani na ya kigeni, kama sehemu ya uchunguzi kuhusu upatikanaji wa fedha kinyume na sheria kwa mashirika hayo, ulifanywa kwa mujibu wa sheria. Watu kadha wametakiwa kufika mahakamani kwasababu kunaonekana kuwa na ushahidi wa kutosha. Miongoni mwao ni Wamarekani 19, hali iliyosababisha maseneta watatu wa Marekani kuionya Misri kuwa inajiweka katika hali ya kuvuruga uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Baraza la mawaziri la serikali ya Ujerumani limeunda tume ya watu wanne ya majimbo itakayoshughulikia mauaji yaliyofanywa na Wanazi mamboleo. Tume hiyo itafanya kazi kwa pamoja na vyombo vya usalama vya majimbo na taifa, na suala kuu likiwa ni kulilenga kundi la wanazimamboleo la Zwickau. Msingi wa tume hiyo utakuwa katika matokeo ya ripoti ya uchunguzi iliyowasilishwa katika bunge la Ujerumani, Bundestag, na bunge la jimbo la Thüringer. Wanazimamboleo wamehusika katika mauaji ya watu tisa ambao ni wafanya biashara wadogo, wenye asili ya Uturuki na Mgiriki mmoja pamoja na polisi mwanamke mmoja. Suala kuu ni kwanini maafisa wa idara za usalama wa taifa walishindwa kuwagundua watu hao waliofanya uhalifu huo ambao ni wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times , miezi miwili baada ya kuondoa majeshi yake kutoka Iraq, Marekani inapanga kuchukua hatua nyingine muhimu ya kupunguza kwa kiasi kikubwa ujumbe wake wa kidiplomasia nchini humo. Katika ubalozi wa Marekani mjini Baghdad kwa hivi sasa kuna wafanyakazi 16,000, wanadiplomasia 2,000 na wafanyakazi wa kawaida 14,000, na huenda nusu yao wakaondolewa. Sababu ya kuchukuliwa hatua hii ni pamoja na kuvunjika moyo kuhusiana na hali ya mkwamo nchini Iraq dhidi ya ushawishi wa Marekani katika hatua za kidemokrasia nchini humo. Uhusiano usioridhisha hauhalalishi gharama inayofikia kiasi ya dola bilioni sita kwa mwaka ambayo Marekani inakabiliana nayo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni, Victoria Nuland, amethibitisha mpango huo kwamba Marekani inapanga kuuwezesha ujumbe wa kibalozi nchini Iraq kufanyakazi vizuri. Pamoja na hayo haijafahamika bado ni kiasi gani ujumbe huo utapunguzwa.
Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.de.